Zitto Kabwe asema yupo tayari kubebeshwa mzigo

Posted on Aug 2 2012 - 4:20pm by Mwemutsi Erick

Tuhuma za rushwa kuibuka bungeni na baadhi ya wabunge kudaiwa kuhongwa zimemuibua Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe na kusema yupo tayari kubebeshwa mzigo badala ya kuhusisha wabunge ambao ni wajumbe wa kamati yake.

Aidha, Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema),  alisema wananchi wasishangae baadaye kubaini kwamba baadhi ya wanasiasa wenye midomo mikubwa ya kutuhumu wenzao wao ndio vinara wa kupokea rushwa.

Madai ya kuwepo kwa rushwa bungeni yaliibuka katika mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma wakati wa kuchangia bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ambapo ilidaiwa kuwa baadhi ya wabunge walihongwa fedha kwa lengo la kuyatetea makampuni ya mafuta na menejimenti ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco).

Zitto katika taarifa yake aliyoisambaza kwa vyombo vya habari jana na baadaye kuzungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, alisema kuwa zipo hoja pandikizi za kutaka POAC ivunjwe na hasa zikimlenga yeye (Zitto) kama mwenyekiti wa kamati hiyo.

“Kwa maoni yangu, Kamati ya POAC isihusishwe na tuhuma hizi kwa vyovyote vile. Niko tayari nihukumiwe, mimi kama mimi na sio kuhusisha wajumbe wengine ambao hawatajwi mahala popote katika tuhuma hizi mbaya sana katika historia ya Bunge letu,” alisema Zitto.

Alisema wapo watu wenye kiu, wasioitakia mema Tanzania kuiona POAC ikivunjwa au sura zikibadilishwa kwa kuwa kamati hii imekuwa mwiba kwa mikakati yao ya kifisadi.

Zitto, alisema atakuwa tayari kuinusuru POAC isivunjwe kwa maslahi ya Taifa kwa kuchukua uamuzi mgumu wa kujiuzulu uenyekiti iwapo itathibitika pasipo shaka kuwa amehongwa hasa ikizingatia kuwa kamati hiyo ni muhimu zaidi kuliko yeye (Zitto).

Alisema anafahamu kuwa kuna wanasiasa hasa wa upinzani ambao wanautaka sana uenyekiti wa POAC na wanafanya kila njia kutaka kuidhoofisha, lakini hawajui kuwa anayepanga wajumbe wa kamati ni Spika wa Bunge.

“Ni lazima tufike mahali kama viongozi kwamba utaratibu unapokiukwa na yeyote yule, au uongo unapotolewa hadharani tuseme bila kuogopa. Hili ndio jukumu letu kama wabunge na viongozi,” alisema Zitto.

Alisema taarifa za rushwa dhidi yake kama kawaida ya uzushi mwingine wowote  zimesambazwa kimkakati na kwa kasi kubwa kiasi cha kuukanganya umma.

Aliongeza kuwa anafahamu kuwa anabeba dhamana kubwa ya uongozi, taswira yake ya uongozi daima imeakisi njozi na matumaini ya wananchi wa Kigoma Kaskazini, wananchi wanyonge na vijana kote nchini bila kujali itikadi zao za kisiasa, jinsia zao, makabila yao na rika zao.

“Nawajibika kupitia kwenu kuwatoa hofu juu ya hisia potofu zinazopandikizwa kwao na wale wasiopenda kuona baadhi yetu tukiwaunganisha na kuwasemea Watanzania wasio na sauti, dhidi ya vitendo vya hujuma na vyenye dhamira ovu kwa taifa,” alisema Zitto.

Alisema mkakati wa kumuunganisha na baadhi ya wabunge wanaotuhumiwa kwa kupokea rushwa unatekelezwa kutokana na kuwepo kwa kauli za watendaji wa serikali ambao wamekuwa wakizieneza na hususan kutoa taswira kwamba baadhi ya kauli zake (Zitto) zinatokana na ushawishi wa rushwa.

Alisema baada ya Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco chini ya uenyekiti wa Meja Jenerali Mstaafu Robert Mboma kutangaza kuwasimamisha viongozi wa Tanesco, POAC ilimuandikia Spika kumuomba aridhie ili kamati iweze kuiita bodi hiyo.

Alisema wengine walioombwa kuitwa na kamati hiyo ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali  (CAG) na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) ili kujiridhisha na tuhuma zote zinazotajwa zinafanyiwa uchunguzi wa kina na hatua kuchukuliwa.

Alisema kamati kujiridhisha na hatua za bodi ni sehemu ya msingi ya utekelezaji wa majukumu ya kamati yaliyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge na pia Tanesco ni moja kati ya mashirika ambayo yanawajibika kwa kamati yake kwa hesabu zake na pia ufanisi wake kwa ujumla.

Hata hivyo, alisema yupo tayari kuchunguzwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Chama chake cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na vyombo vya dola na ikiwa itathibitika amepokea rushwa atawajibika kisiasa.

“Sina bei, sijawahi kuwa nayo na sitarajii kuwa nayo huko mbeleni…ninawaahidi sitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa katika nchi hii pamoja na mikakati ya aina hii ya kunidhohofisha na kunivunja moyo,” alisema.

Zitto alisema kamati yake inasimamia mashirika 259 ya umma na kwamba wanaoibua tuhuma za rushwa dhidi yake ni kutaka kuivuruga kamati hiyo ili kufanikisha nia ya wanaotaka kukidhi kiu ya tamaa zao za kupora rasilimali za nchi.

Alisema hakuna sababu ya kuihusisha POAC na tuhuma zinazoelekezwa kwake na badala yake alitaka ahukumiwe yeye binafsi na anasubiri uchunguzi ambao kama utathibitisha tuhuma hizo atajiuzulu nafasi ya uenyekiti kwenye kamati.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Zitto aliongozana na wabunge wengine wa chama chake ambapo pia aliwatuhumu wabunge wa upinzani kwamba wanataka POAC ivunjwe ili warithi nafasi yake ya uenyekiti.

Wakati huo huo, Zitto amesema serikali imeingia mkenge mwingine wa kulipa ‘capacity charge’ ya Sh. milioni 152 kila siku kwa Kampuni ya Symbion ambayo ilinunua iliyokuwa mitambo ya Richmond/Dowans fedha zinazolipwa hata kama kampuni hiyo haizalishi umeme au la.

Kadhalika, alisema kuwa Tanesco linatumia Sh. bilioni 42 kwa mwezi kulipa gharama mbalimbali kwa makampuni ya Songas, Aggreko na IPTL ikiwemo kununua mafuta mazito ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme wa kampuni hizo.

Zitto alisema gharama hizo zinachangia kuidhohofisha Tanesco kiutendaji na kifedha.

Alisema malipo hayo yanatokana na mikataba ya kinyonyaji baina ya serikali/Tanesco na kampuni hizo ambayo imekuwa ikipigiwa kelele na wabunge kwa muda mrefu bila mafanikio.

Alisema inashangaza kuona Symbion ikilipwa mamilioni ya fedha kila siku; miezi michache baada ya serikali na wanasiasa wenzake kupinga wazo lake la kutaka serikali inunue mitambo ya Dowans ili iweze kuzalisha umeme wa gesi ambao ungeuzwa kwa gharama ndogo kwa wananchi.

Zitto alisema taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Tanesco inaonyesha kwamba shirika hilo limekuwa likitumia asilimia 86 ya mapato yake kulipia gharama kwenye kampuni zinazozalisha umeme, hali ambayo inatokana na mikataba ya kinyonyaji.

Alisema ni katika kupinga ufisadi huo kumepelekea yeye (Zitto) kuzushiwa kwamba amepokea rushwa ili atetee mafisadi wanataka kuihujumu Tanesco.