Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Ajiuzulu

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Hamad Nassoro, ameamua kujiuzulu kufuatia ajali ya meli ya MV Skagit iliyozama na kuua watu 73 na wengine 72 kupotea Julai 18, mwaka huu.

Akihojiwa na kituo cha Televisheni cha Channel Ten jana usiku, Waziri Hamad alisema tayari alimwandikia barua Rais Dk. Ali Mohammed Shein kuhusu suala hilo tangu Julai 20, mwaka huu na tayari amemteua Rashid Seif Suleiman kushika nafasi yake.

Alisema uamuzi huo haukutokana na shinikizo la mtu yeyote bali ameona ni busara kwa kiongozi wa kisiasa kuchukua hatua hiyo kwa lengo la kumrahisishia kazi Rais.

“Hakuna shinikizo lolote na si lazima nisubiri tume, nimeamua mwenyewe kujiuzulu ili kumrahisishia Rais,” alisema.

Wakati hayo yakitokea, meli ya MV Skagit imebainika kwamba ilitengenezwa nchini Marekani kwa matumizi ya vivuko na sio kusafirisha abiria masafa marefu kama  ilivyokuwa ikitumika Zanzibar.

Hayo yalieleezwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu zoezi la uokozi tangu kutokea kwa ajali hiyo Julai 18, mwaka huu.

Alisema kampuni ya Seagull Sea Transport Limited ilinunua boti hizo mbili ikiwemo ya MV Kalama na MV Skagit na kusajiliwa Zanzibar Oktoba 25, mwaka jana na Mamlaka ya Usafirishaji Zanzibar (ZMA).

Alisema zilipewa namba ya usajili 1000144 kabla ya kuanza kutoa huduma katika visiwa vya Zanzibar na Tanzania Bara.

Alisema wakati zinatengenezwa kiwandani mwaka 1989, matumizi yake yalikuwa ni kutoa huduma katika vivuko vyenye umbali wa kilomita saba na siyo kusafirisha abiria masafa marefu na kwamba ilikuwa imebakisha miaka miwili kumaliza muda wake wa matumizi kwa huduma za vivuko.

“Meli hizi zilitengenezwa kwa matumizi ya usafiri wa kivuko siyo kusafirisha abiria masafa marefu kama ilivyokuwa zikitumika Zanzibar,” alisema.

Kwa msingi huo, alisema serikali imepiga marufuku kutoa huduma boti ya MV Kalama.

Balozi Idd alisema Serikali imeamua kuunda tume ya kuchunguza ajali hiyo ili kupata ukweli na kuangalia hatua za kuchukua kama kulikuwa na mazingira ya ajali kabla ya kuchukua hatua za kisheria kwa wahusika.

Alisema katika ajali hiyo, kulikuwa na raia wa kigeni 17 kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Ubelgiji, Marekani, Ujerumani, Uholanzi na Israel.

Alisema zoezi la kutafuta meli hiyo bado halijapata matumaini makubwa ya kuonekana licha ya wazamiaji kuzamia umbali wa mita 48 ya kina cha bahari.

Aliwataka wananchi ambao wamepotelewa na jamaa zao kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali za mitaa, masheha, wakuu wa wilaya na vituo vya Polisi Zanzibar na Tanzania bara.

“Serikali imehuzunishwa sana na tukio hili imekusudia kuchukua hatua ikiwemo kuunda tume ya uchunguzi wa ajali hiyo,” alisema Balozi Iddi.

Aidha, alisema serikali inatarajia kuzifanyika mapitio sheria zinazohusu usafiri wa baharini na kuweka viwango vya aina ya meli zitakazoruhusiwa kuingizwa nchini na kuchukua abiria.

Alisema sheria mpya itaweka masharti magumu ikiwemo watu kuingiza boti mpya au zilizotumika miaka 15 kabla ya kumaliza muda wake.

“Hatutaki kuona Zanzibar inaendelea kuwa jalala la meli mbovu, tumeamua kupitia upya sheria ya usafirishaji Zanzibar,” alisema.

Hata hivyo, alisema meli hiyo ilikuwa na abiria 290 wakiwemo watoto 31 mabaharia 9, lakini hadi jana maiti 73 zilikuwa zimepatikana, wakiwemo watoto 17 wanawake 37 na wanaume 19.

Alisema watu 72 bado kuonekana na kuwataka wananchi kutoa taarifa iwapo wataona maiti katika maeneo yoyote ya Zanzibar.

Balozi Iddi alisema kutokana na maiti hizo kuharibika, serikali imeamua kuzika kila zinapopatikana na kuweka kumbukumbu za kusaidia wahusika kupata taarifa za watu wao.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Zanzibar limesema mmiliki wa meli hiyo na nahodha wanatarajia kufikishwa mahakamani leo kujibu mashitaka yao kufuatia kuzama kwa boti hiyo.

Kamishna wa jeshi hilo, Mussa Ali Mussa, alisema kazi ya uchunguzi inaendelea vizuri na tayari jalada la mashitaka limekabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP) kabla ya wahusika kupandishwa kizimabani leo.

Alisema nahodha wa meli hiyo Mussa Makame Mussa, mmiliki Said Abdulrahman na Meneja wake Omar Hassan Mkonje, wamehojiwa na makachero wa jeshi la polisi Zanzibar.

Wazamiaji katika ajali hiyo tayari wamesema zoezi la utafutaji wa meli limekwama baada ya kukosekana kifaa cha kusaidia kutambua chuma chini ya bahari au Alumium kitwacho ‘Flash Diver Founder’ ambacho hakipatikani Afrika Mashariki.

Mzamiaji Ali Ramadhani, alisema kifaa hicho kina umuhimu mkubwa lakini vikosi vya uokozi Tanzania bara na Zanzibar hawana ndiyo maana wameshindwa kuiona meli kutokana na kuzama katika mkondo mkubwa wa bahari.

Add a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

`
Design By : Tanzania Servers Technology