WASTARA APATA FURAHA NA MACHUNGU KWA PAMOJA

Wastara Juma

Safari ya maisha ya muigizaji wa sinema za Kibongo, Wastara iligubikwa taswira ya faraja kidogo huku machungu pia yakichukuwa nafasi yake.
Wastara alizaliwa Septemba 27, mwaka 1983 huko mkoani Morogoro. Mwaka 1987 akajiunga na Shule ya Msingi Mvomelo ‘A’ na kufanikiwa kumaliza elimu yake ya msingi mwaka 1995.
Mkali huyo kipenzi cha watu kwenye ulingo wa sanaa, mwaka 1996 alijiunga na Sekondari ya Agricalture mkoani humo ambapo hakufanikiwa kumaliza kidato cha nne kutokana sababu zilizokuwa nje ya uwezo wake.
“Kuna rafiki yangu alikuwa anakula fedha za dada yake sasa tukawa tunatumia naye sasa msako ulipofanyika mimi nikaonekana ndiyo chanzo cha wizi huo mkubwa wa fedha ikabidi nitimke zangu,” anasema Wastara.
ATIMKIA MLANDIZI
Kwa kuwa darasa halikuendelea, Wastara aliamua kurudi Mlandizi mkoani Pwani kwa bibi yake aliyekuwa akiishi maeneo hayo miaka hiyo ya 1996 baadaye kurudi tena Morogoro kusomea masuala ya madini.
Lengo la kusomea fani hiyo lilikuwa ni kumsaidia bibi yake aliyekuwa akifanya biashara ya kuuza madini mara atakapohitimu.
Mwaka 1997, mwigizaji huyo alifanikiwa kupata mume, kwa mara ya kwanza akaolewa na jamaa mmoja aliyejulikana kwa jina la Juma Issa ambapo mwaka 1998 alibahatika kuzaa naye mtoto mmoja kisha ndoa hiyo ikasambaratika kutokana na kutofautiana kwa tabia.
AKUTANA NA MAJUTO
Mara baada ya kumwagana na Juma, mwaka 1999 Wastara alianza kuvutiwa na uigizaji baada ya kuona kazi mbalimbali alizokuwa akizifanya mwigizaji wa kitambo, Athuman Majuto ‘King Majuto’.
Aliamua kufunga safari hadi mkoani Tanga kwa ajili ya kusaka nafasi ya kuigiza, alipofika mkoani humo, bahati nzuri alimkuta mzee Majuto akiwa katika harakati za kuanza kurekodi filamu ya Utaishia Kunawa. Mzee Majuto alivutiwa na muonekano wake, moja kwa moja akamuamini acheze filamu hiyo tena kwa nafasi ya mhusika mkuu.
“Kwa kuwa nilikuwa nikipenda anavyoigiza (Majuto), nilitamani kuigiza vizuri ili niendelee kuigiza naye na kweli nikafanikiwa kufanya vizuri sana kwenye filamu hiyo,” anasema Wastara.
Mara baada ya filamu hiyo kutoka, wazazi wa Wastara walimjia juu kwa kudai filamu ni mambo ya kihuni na kumtaka aache mara moja, akaacha.
AIBUKIA ITV
Baada ya kujiibaiba mara kwa mara kuigiza bila mafanikio makubwa, hatimaye mwaka 2006 staa huyo wa filamu aliibukia kwenye mikono ya Kundi la Sanaa za Maigizo la Kaole.
Hapo akaanza kuuza sura katika mchezo wa Miale ambapo ulimpa umaarufu zaidi baada ya kuonesha umahiri wake wa kuigiza.
AKUTANA NA JENIFA MGENDI
Wastara hakudumu sana kwenye kundi hilo, alikutana na kina Jenifa Mgendi ambaye pia walifanikiwa kuigiza naye filamu iliyowashirikisha baadhi ya wasanii wa kitambo akiwamo Dino na wengineo.
Mwaka 2007, Wastara alifanya usahili kwenye filamu ya mdau Ande John iliyofahamika kama Pelemende, akafaulu na kuigiza kwenye filamu hiyo kisha zikafuata filamu nyingine kama Penina kabla ya kutimkia nchini Kongo kufanya biashara.
AKUTANA NA SAJUKI
Aliporejea kutoka Kongo, Julai, 2007, Wastara aliitwa na mwigizaji Shija ambaye alimuomba aigize naye filamu baada ya kumuona kupitia kazi mbalimbali alizowahi kufanya hapo nyuma.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa Wastara kukutana na Sajuki ambaye sasa ni mumewe wa ndoa kwani Shija alikuwa akifanya kazi zake za uigizaji kwa kupata msaada mkubwa kutoka kwa Sajuki.
Wastara alicheza filamu kadhaa akiwa na Shija pamoja na Sajuki hadi baadaye walipokuja kugundua kuwa matatizo ya uhusiano yaliyowakuta (Sajuki na Wastara) yanafanana kwani kila mmoja wao alitendwa na mpenzi wake ndipo walianzisha uhusiano wa kimapenzi.
“Eeeeh! Kazi na dawa, tuligundua kuwa matatizo yetu yanafanana. Taratibu tukaanza uhusiano ili kufarijiana,” anasema Wastara.
FILAMU WALIZOZALISHA
Wakiwa ndani ya umoja wao, Sajuki na Wastara, walifanikiwa kuporomosha filamu kama Mboni Yangu, Two Brothers ambazo zilifanya vizuri sokoni.
APATA AJALI
Wakati harakati za ndoa zikiwa zimepamba moto, mwaka 2009 Wastara alipata ajali ya pikipiki iliyosababisha akatwe mguu.
Wakati huo tayari alikuwa ameshachumbiwa na Sajuki.
Juni mwaka huohuo,
wasanii hao waliopitia changamoto kadhaa za maisha, walifunga ndoa na kuanza rasmi maisha ya mume na mke.
Baada ya hapo, kupitia kampuni yao ya Wa-Jey waliendelea kuzalisha filamu kama Briefcase, The Killers, Seven Days na Mboni Yangu.
APATA MTOTO
Pamoja na kumuuguza mumewe anayesumbuliwa na ugonjwa wa uvimbe tumboni hadi sasa, mapema mwaka huu Wastara alijifungua mtoto Farheen katika Hospitali ya TMJ jijini Dar.
MAFANIKIO
Kwenye sanaa, Wastara amefanikiwa kujulikana na watu wengi kutokana na filamu zake zenye hisia, usafiri wa kutembelea pamoja na nyumba iliyopo Tabata jijini Dar.

Add a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

`
Design By : Tanzania Servers Technology