Wanafunzi DIT wagomea mitihani

Posted on Jun 3 2014 - 1:10pm by Mwemutsi Erick

Wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) wamegoma kufanya mitihani ya muhula kutokana na wenzao 684 kutopatiwa namba za mitihani kwa madai ya kutokamilisha usajili.

Mgomo huo umesababisha mitihani iliyopangwa kufanyika jana asubuhi na mchana kutofanyika kutokana na wanafunzi hao kugomea kuingia vyumba vya mitihani.

Akizungumza na NIPASHE Rais wa serikali ya wanafunzi, Himida Elihuruma, alisema wamelazimika kugomea mitihani hiyo kwa sababu kuna wanafunzi walifanya usajili tangu Februari, lakini hawajapewa namba za mtihani kwa maelezo kuwa hawajakamilisha taratibu.

“Kuna wanafunzi wamesajiliwa baada ya kukamilisha taratibu zote tangu Februari, lakini  la kusikitisha hawajapatiwa namba kwa kuambiwa kwamba hawajafanya usajili,” alisema Elihuruma.

“Ofisi ya Uhasibu imegubikwa na rushwa, kuna ushahidi wa baadhi ya viongozi na wanafunzi waliombwa ili watafutiwe fomu ambazo zimepotea hali iliyopelekea hadi leo kutopata namba za mtihani,” alisema.

Aidha, alisema kumekuwapo na ubaguzi unaofanywa na utawala kwa kuwanyima namba za mitihani wanafunzi waliokamilisha usajili na kuwapa ambao hawajakamilisha. Aliongeza kuwa uongozi wa chuo umekuwa na utaratibu mbovu wa kupanga tarehe za usajili na kwa mara ya kwanza ilipangwa Machi 7  ikasogezwa Mei 16 hadi 23, mwaka huu bila kutoa taarifa kwa wanafunzi.

Wanafunzi waliohojiwa na gazeti hili walisema hawatafanya mitihani hiyo hadi pale wenzao watakapopewa namba.

Ofisa Uhusiano wa taasisi hiyo, Amani Kakana, alisema mgomo huo hautambuliki na mitihani iliyogomewa jana itapangwa tena na usajili hautaongezewa muda.

“Tulitoa muda wa kutosha wanafunzi kufanya usajili walioshindwa kufanya kwa wakati hawawezi kupatiwa namba, tunafuata utaratibu wa chuo uliopangwa unaoleweka na wanafunzi,” alisema Kakana.

“Mwanafunzi anayejielewa hawezi kugomea mtihani, ratiba haitaharibika itaendelea kama ilivyopangwa, tutamchukulia hatua kali mtu yeyote atakayejaribu kuchochea vitendo vya uvunjifu wa amani,” alisema.