Wabunge: APEX inanyonya wakulima

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Chistopher Chiza

Wabunge wamekishambulia vikali Chama Kilele (Apex), cha kusambaza pembejeo kwa wakulima nchini na kuitaka serikali kukifutilia mbali kutokana na sababu kadhaa ikiwamo ya kuwanyonya wakulima.

Wabunge hao walitoa mashambulizi hayo bungeni jana wakati wakichangia Muswada wa Sheria wa Vyama vya Ushirika wa mwaka 2013.

Walisema hakuna sababu ya kuendelea kuwa na Apex kwa kuwa kimeonyesha dhahiri kushindwa kabisa kuwasaidia wakulima zaidi ya kuwanyonya huku viongozi wake wakiwa ni matajiri wa kutupwa wa kujilimbikizia mali.

Magdalena Sakaya (CUF-Viti Maalum), alisema Apex ni mnyonyaji mkubwa wa wakulima huku viongozi wake wakiwa wamejilimbikizia mali zinazotokana na jasho la wakulima na kuwa imekuwa ikisambaza mbolea kwa gharama kubwa  na kuchelewesha soko la mazao kwa makusudi ili baadaye iuze kwa gharama kubwa.

Alisema wapo baadhi ya wabunge wamekula mlungula (rushwa) kupitia Apex. Hata hivyo, hakufafanua zaidi.

Dk. Pudenciana Kikwembe (CCM-Viti Maalum), alisema ametumwa na wakazi wa Mkoa wa Katavi alieleze Bunge kuwa hawataki kusikia wala kuona kitu ama watu wanaoitwa Apex na kuwa imechangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya wakulima mkoani Katavi kutokana na kuwapelekea mbolea kwa wakati usio mwafaka.

Sabrina Sungura (Chadema-Viti Maalum), alisema anakubaliana na wabunge wenzake kutaka Apex iondolewe kwakuwa imekuwa ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya wakulima.

Naye Mbunge wa Mtambile (CUF), Masoud Abdallah Salum, alisisitiza kuwa ni muhimu Apex ikaondolewa ili  wakulima wapate haki zao pasipo kunyonywa. Mbunge wa Namtumbo (CCM), Vita Kawawa, alisema hakuna sababu ya kuendelea kuwa na Apex kwa kuwa imeshindwa kuwafikishia wakulima mbolea kwa wakati mwafaka na kwa bei wanayoweza kumudu.

Hata hivyo, Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Hamis Kigwangwalla, alisema tatizo si Apex bali ni uongozi na usimamizi.

Hata hivyo, wakati wa kujibu hoja za wabunge, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Chistopher Chiza, aliahidi kuwa serikali itaifuta Apex.

Add a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

`
Design By : Tanzania Servers Technology