Mbunge aliyevamiwa ataka Polisi waongezewe vitendeakazi

Prudenciana Kikwembe

Serikali imeombwa kuliongezea vitendea kazi Jeshi la Polisi ili liweze kukabiliana na vitendo vya uhalifu hapa nchini.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mbunge waViti Maalum (CCM), Prudenciana Kikwembe, kufuatia tukio la kuporwa fedha na kadi za benki juzi katika baa ya Lady May Pub.

Kikwembe alisema hali hiyo imetokana na kusuasua kwa kwa utendaji kazi wa askari kuchelewa kufika katika maeneo ya matukio mbalimbali ikiwemo tukio la kuporwa kwake.

Alisema mara nyingi watu wamekuwa wakilitupia lawama jeshi la polisi lakini utendaji wao umeonekana ni dhaifu kutokana na kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha.

Mbunge huyo alisema katika tukio lake lililotokea Aprili 25, mwaka huu alivamiwa na mtu anayesadikiwa kuwa ni jambazi na kuporwa mkoba wenye dola za Marekani 600 pamoja na Sh. 180,000 majira ya saa mbili usiku na sio saa nane kama ilivyoripotiwa awali.

Akizungumzia tukio hilo, alisema lilitokea majira ya saa mbili usiku na kutokana na hali ya woga walijifungi ndani ya nyumba hiyo na kujaribu kupiga simu polisi kupitia namba 112  lakini haikuwa na mafanikio yoyote.

Alisema wakati wakijadili wafanye nini ndipo akapata wazo la kumpigia ndugu yake ambaye ni askari anayeishi Kikuyu manispaa ya Dodoma aliyemtaja kwa jina la Faraja ili kumueleza tukio hilo.

Alifafanua kuwa baada ya kumweleza Faraja akatoa taarifa polisi majira ya saa nane usiku ndipo askari wakafika eneo la tukio.

Aidha alisema eneo hilo la tukio lipo pia jirani na kituo kikuu cha polisi mkoani hapa lakini askari hawakuweza kusikia mlio wa risasi ili kufuatilia ni wapi.

Alisema hali ya jeshi la polisi la kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha ni hatari kubwa kwa wananchi wa kawaida kwani wanaweza kuathirika zaidi pindi panapotokea uvamizi.

Hata hivyo, alisema atamuhudumia kijana Ally Kibula(22), ambaye amelazwa kwenye hospitali ya mkoa wa Dodoma kwa matibabu kutokana na kujeruhiwa kwa risasi wakati wa tukio la uporwaji.

Mbunge huyo alivamiwa Aprili 25 na mtu ambaye bado hajajulikana katika eneo la barabara ya Iringa karibu na baa ya Lady May Pub na kuporwa vitu mbalimbali ukiwemo mkoba uliokuwa na dola 600 za Marekani, Sh. 180,000 pamoja na kadi za benki.

Kwa upande wa majeruhi huyo, Kibula alisema anaendelea vizuri kidogo lakini mguu bado unauma sana.

Alisema picha ya X-Ray inaonyesha mfupa haujavunjia ilipokuwa vipande vya risasi vilisambaa katika mguu huyo na kwasasa vimetolewa.

Add a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

`
Design By : Tanzania Servers Technology