LULU (Elizabeth michael) Kufikishwa kortini wakati wowote

Elizabeth Michael ''LULU"

Msanii nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba amefariki dunia kwa kile kinachodaiwa kuibuka kwa ugomvi kati yake na mpenzi wake .

Kufuatia kifo hicho, Jeshi la polisi mkoa wa Kinondoni, linamshikilia mcheza filamu nchini Elizabeth Michael maarufu kama ‘Lulu’ ambaye ni mpenzi wa msanii nyota huyo.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Charles Kenyela, alithibitisha kushikiliwa kwa msanii huyo na kueleza kuwa mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi kukamilika.

Kamanda Kenyela aliliambia Kwetu Bongo Jumapili jana kuwa, taarifa za kifo cha msanii huyo wa filamu nchini, walizipokea kupitia kwa mdogo wa marehemu aliyekuwa akiishi nyumbani kwa Kanumba eneo la Sinza Vatican.

Alisema ndugu huyo wa marehemu ambaye jina lake hakulitaja, aliijulisha polisi kuwa, hali ya msanii huyo ni mbaya baada ya kutokea ugomvi kati ya Kanumba na mpenzi wake.

Kenyela alisema kwa mujibu wa ndugu huyo, majira ya saa 9:00 usiku alisikia wawili hao wakigombana chumbani kwao bila kujua sababu ya ugomvi.

Alisema baada ya dakika kadhaa mpenzi huyo alitoka na kuondoka ndipo ndugu huyo alipoingia chumbani kwa kaka yake na kukuta akiwa hajitambui.

Kenyela alisema baada ya polisi kufika nyumbani hapo walimkuta msanii huyo akiwa hajitambui huku mazingira ya chumba yakiwa ya kawaida na hapakuwa na silaha yoyote.

Hata hivyo, Kenyela alisema upelelezi wao wa awali umeonyesha kuwa, chanzo cha kifo hicho kimesababishwa na hali ya kutoelewana iliyosababisha kuibuka kwa ugomvi.

“Tunahisi huyu mwanamke katika kujihami labda alimsukuma Kanumba au alitumia kitu kizito kumpiga wakati amelala, ila tunasubiri uchunguzi kamili kutoka kwa daktari ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa,” alisema.

Aliongeza kuwa, baada ya ugomvi mwanamke huyo aliondoka eneo la tukio na alikamatwa mtaani kati ya saa 2:00 na saa 4:00 asubuhi.

Alisema mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakati upelelezi wa tukio hilo ukiendelea.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria kwenye msiba wa marehemu Kanumba na kutia saini kitabu cha maombolezo ni pamoja na mke wa Waziri Mkuu, Tunu Pinda, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Mbunge wa Kinondoni Iddi Azzan, Katibu Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na Ridhiwani Kikwete

Pia Meya wa Manispaa ya Kinondoni na Ilala, Yusuf Mwenda na Jerry Slaa ni miongoni mwa viongozi waliojitokeza kwenye msiba wa Kanumba aliyefariki juzi usiku nyumbani kwake baada ya kuanguka katika mzozo na mpenzi wake.


RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI

Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), kuomboleza kifo cha msanii Kanumba, aliyeaga dunia usiku wa kuamkia jana.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana kwa vyombo vya habari ilisema Rais Kikwete amemuomba kiongozi wa TAFF kufikisha salamu za rambirambi za dhati ya moyo wake kwa wana-familia ya Kanumba na kwa wasanii wote nchini ambao wamepotelewa na mdau mwenzao.

Rais Kikwete amesema kuwa ameshtushwa na kuhuzunishwa na kifo cha msanii huyo ambaye amemwelezea kuwa ni msanii mahiri na mwenye kipaji kikubwa ambaye katika uhai wa maisha yake mafupi na akiwa bado kijana sana amechangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya sanaa ya filamu nchini na kupitia sanaa hiyo kuitangaza Tanzania kimataifa.

Nimepokea kwa mshtuko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ndugu Steven Charles Kanumba. Kupitia filamu zake, ameburudisha na kuelimisha jamii yetu kwa namna ambayo haiwezi kupimika. Alikuwa msanii mahiri na mwenye kipaji kikubwa ambaye mchango wake mkubwa katika kuanzisha, kukuza na kuimarisha sanaa ya filamu nchini hautasahaulika.”

“Ndugu Kanumba pia ametoa mchango mkubwa katika kuitangaza nchi yetu ya Tanzania mbele ya mataifa mengine kupitia sanaa ya filamu na uwezo mkubwa wa kisanii. Tutaendelea kumkumbuka kwa mchango wake huo kwa nchi yetu.”

“Nakutumia wewe Rais wa TAFF salamu zangu za rambirambi na kupitia kwako kwa wasanii wote wa filamu na sanaa nyingine kufuatia msiba huu mkubwa kwa fani yetu ya sanaa. Aidha, naomba unifikishie salamu za dhati ya moyo wangu kwa wanafamilia wote. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa. Waambie naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu cha msiba,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Namwomba Mwenyezi Mungu awape subira na nguvu za kuweza kuhimili kipindi hiki kigumu kwa sababu yote mapenzi yake. Aidha, naungana na wana-familia na wasanii wote nchini kuwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema peponi roho ya Marehemu Steven Charles Kanumba. Amen.”

UMATI WAJITOKEZA MSIBANI

Umati mkubwa uliojitokeza kwenye msiba wa msanii huyo uliopo nyumbani kwake Sinza Vatican, jana ulisababisha msongamano mkubwa kiasi cha kuziba barabara ya Makanya na kuwalazimisha askari polisi kufanya kazi ya ziada ya kuelekeza watu.

Mwandishi wa KwetuBongo Jumapili aliyekuwepo msibani hapo, alishuhudia umati mkubwa wa watu wakiwemo viongozi wa Jiji la Dar es Salaam, Meya wa Ilala, Slaa, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika, Katibu wa Kamati ya Uchumi na Fedha CCM-Taifa, Mwigulu Nchemba na Diwani wa Kata ya Sinza, Renatus Pamba wakiwafariji wafiwa.

Kutokana na wingi wa watu waliojitokeza kwenye msiba huo, iliwalazimisha waratibu wa msiba huo, kuwahamisha waombolezaji hao kwenye ukumbi wa Vatican Hoteli, huku wakiwazuia wengine kuingia ndani na kuleta tafrani za hapa na pale.

Mratibu wa Bongo Movie, Steven Mengele ‘Steve Nyerere’ alisema waliamua kuhamishia watu hotelini hapo kutokana na eneo la nyumba ya marehemu Kanumba kutotosha kwa wingi wa waombolezaji waliojitokeza waliosababisha msongamano mkubwa.

Msongamano huo wa waombolezaji ulisababisha hata magari yanayotumia barabara ya Makanya kushindwa kupita na kuwapa kazi ya ziada askari polisi wa kawaida na wale wa barabarani kuyaongoza magari hayo.

Wasanii mbalimbali walikielezea kifo cha Kanumba kama pengo litakalochukua muda mrefu kuziba katika tasnia ya sanaa hasa uigizaji wa filamu ambayo marehemu aliifanya kwa muda mrefu wa maisha yake tangu akiwa shuleni.

Msanii Yvone Sherry maarufu kama Monalisa, alilia kwa huzuni hasa ikizingatiwa kuwa hivi karibuni walikuwa nchini Ghana na marehemu Kanumba wakitayarisha filamu yao mpya.

“Nimeumbuka mimi, Kanumba umeniacha wakati tulikuwa tukijiandaa kwenda kwenye filamu za kimataifa,” alilia Monalisa kwa huzuni.

Mlimbwende Wema Sepetu, ambaye alikuwa na mahusiano na marehemu Kanumba, alisema ni wiki moja iliyopita alipokutana naye na kutaniana naye. Amesema kifo chake amekipokea kwa mshituko mkubwa.

Mayasa Mrisho anayefanya kazi nyingi na Kanumba, alisema mpaka sasa haamini kama Kanumba kafariki kwa namna kifo chake kilivyokuwa cha ghafla.

“Siamini, kama ni kweli Kanumba kafa,” alisema huku akilia. Aliongeza Kanumba amefariki wakati wakitoka kumalizia kazi yao mpya iitwayo ‘Mr Price’, huku pia wakijiandaa kuingiza sokoni filamu yao mpya iitwayo ‘Ndoa Yangu’.

Wasanii wengine kama Patcho Mwamba, Rajabu Jumanne ‘Chilli’, Issa Kipemba, Fatuma Makongoro ‘Bi Mwenda’ walisema itawachukua muda mrefu kumsahau mwenzao ambaye alikuwa mtu wa watu, asiye na makuu licha ya umaarufu mkubwa aliokuwa nao.

Nalo Baraza la Sanaa la Taifa, kupitia Katibu Mkuu wake, Ghonce Materego, walitoa salamu za rambirambi kutokana na kifo hicho cha Kanumba wakidai kimeshtua na kuwaachia pengo kubwa katika fani ya sanaa nchini.

“BASATA inaungana na familia za wafiwa na wasanii wote nchini kwa maombolezo ya msiba huu mkubwa na wa kihistoria. Kufiwa na msanii huyu mahiri kwenye tasnia ya filamu ni pengo kubwa kwa familia, Sekta ya sanaa na Taifa kwa ujumla kutokana na ukweli kuwa, aliweza kuutangaza utamaduni na sanaa yetu nje ya mipaka,” sehemu ya rambirambi hiyo ya Basata inasomeka hivyo.

Kanumba, alisoma Shule ya Msingi Bugoyi na Shule za Sekondari Mwadui, Dar Christian Seminary na Jitegemee kabla ya kuanza kutamba kwenye sanaa kupitia kundi la sanaa alilojiunga nalo mwaka 2002 hadi 2006 alipojiengua na kucheza filamu mbalimbali.

Baadhi ya kazi zake ni She is My Sister, Dar to Lagos, Cross My Sin, The Director, Hero of the Church, Sikitiko Langu, Dangerous Desire, Dar to Lagos, Cross My Sin, Village Pastor, Family Tears, Unfortunutes Love, My Valentine, The Shock, Deception na kazi ya mwisho kuitoa sokoni ni ‘Kijiji Chatambua Haki’.

Add a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

`
Design By : Tanzania Servers Technology