January Makamba atoa wiki moja kwa TCRA

Posted on Jun 13 2012 - 3:00pm by Mwemutsi Erick

Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia imesema bado haijapokea taarifa yoyote ya utekelezaji wa agizo ililolitoa kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),  la kuzungumza na makampuni ya simu nchini ili yatoe majibu  kuhusiana na matatizo yanayolalamikiwa na wateja dhidi ya makampuni hayo.

Mei 23 mwaka huu, Naibu Waziri wa wizara hiyo, January Makamba, alitoa wiki mbili kwa TCRA kuzungumza na makampuni ya simu ili yatoe majibu kuhusiana na kuwepo kwa matatizo ya huduma za simu na lini yatatatuliwa.

Hata hivyo, akizungumza na NIPASHE jana, Makamba alisema bado hajapewa taarifa kutoka TCRA kama wametekeleza agizo hilo na kwamba anatoa wiki moja tena ili kama bado hawajafanya kazi hiyo waitekeleze haraka.

Makamba ambaye alitoa agizo hilo baada ya kutembelea ofisi za TCRA makao makuu, alisema licha ya kukua kwa sekta ya mawasiliano nchini, lakini kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wateja wanaotumia huduma za simu, kulalamikia huduma hiyo kwamba  mara nyingi imekuwa ikisumbuasumbua.

“Ninaongea kama mwananchi wa kawaida ambaye pia ninatumia huduma hii, licha ya kusikia malalamiko kutoka kwa wananchi, lakini mimi pia ninatumia huduma ya simu, nimeshuhudia kuwepo kwa matatizo ya mitandao hii,” alisema.

“Unaweza kupiga simu ukaambiwa haipatikani hata kama iko hewani, au ukakatwa pesa nyingi tofauti na matumizi, lakini tatizo jingine  ni lile la kutumiwa jumbe nyingi za promosheni,” alisema na kuongeza kuwa haiwezekani makampuni ya simu yakawa yanatumia fedha nyingi katika promosheni pasipo kujali kuweka miundombinu yao vizuri na kuitaka TCRA kuhakikisha matatizo hayo yanashughulikiwa haraka.

Wiki iliyopita NIPASHE ilizungumza na Meneja wa Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy kutaka kufahamu kama utekelezaji huo umefanyika, lakini hakutoa majibu zaidi ya kumtaka mwandishi kumuuliza Makamba akidai kwamba sio utaratibu wa kazi kumjibu waziri kupitia gazetini.

Leave A Response