CUF, CCM Zanzibar washutumiana

Mambo yanaonekana siyo shwari katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumshutumu Waziri wa Sheria na Katiba, Abubakar Khamis Bakari (CUF), kwa kutowajibika na kusababisha vurugu zilizotokea visiwani humo kwa siku tatu na kumtaka ajiuzulu.

Katika tamko lililotolewa kwa vyombo vya habari jana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, lilisema kuwa vurugu zilizojitokeza Zanzibar zimechangiwa na Waziri wa Katiba na Sheria kwa kushindwa kusimamia majukumu yake.

Vuai alisema kwamba vitendo vya uvunjifu wa amani vimeanza kufanyika Zanzibar miezi minne iliyopita na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa licha ya kikundi cha Uamsho kinachohusishwa na vurugu hizo kusajiliwa na serikali.

“Waziri wa Sheria na Katiba ameshindwa kuisaidia serikali, ameonyesha mapungufu makubwa kwa sababu karibu miezi minne Jumuiya hiyo imekuwa ikipandikiza chuki za Wabara na Wazanzibari kwa kutumia jukwaa la dini kwa shughuli za siasa wakiongozwa na chama kimoja cha siasa,” alisema Vuai bila kukitaja chama hicho kwa jina.

Alisema vitendo vilivyofanyika Zanzibar vimeleta athari kubwa kwa watoto, wagonjwa na wanafunzi ambao waliathirika kwa kiwango kikubwa na vurugu hizo.

“Hatuwezi kuwa na Waziri wa Sheria na Katiba ambaye kashindwa kuishauri serikali juu ya katiba na sheria na kuachia uvunjifu wa sheria ukifanyika ndani ya miezi minne, hivyo Waziri Abubakar Khamis Bakari anapaswa kujiuzulu kwa matukio yaliyotokea na hasara zilizopatikana mbali na athari za kiuchumi,” alisema Vuai.

CUF NAYO YATOA KAULI

Wakati CCM ikimtupia lawama Waziri Abubakar, CUF nayo imetoa taarifa kuwelezea msimamo wake kuhusu vurugu za Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa jana na Salim  Bimani, Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu, Habari na Uenezi na Mahusiano na Umma, ilisema: “Umma unashuhudia hali tete ya machafuko ambayo hayakutarajiwa yakiibukia tena Zanzibar, wakati ambapo nchi ilishaanza kunawiri matunda ya utulivu na maridhiano, chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.”

Aliongeza: “Pamoja na sababu au visingizio mbalimbali vilivyotajwa kuwa chanzo cha hali hiyo, zikiwamo hamasa za wananchi, chuki binafsi, ukosefu wa hekima; matumizi ya nguvu za dola, na hata uchochezi wa makusudi wa wale wanaoonekana kutopendelea Maridhiano ya Kisiasa ya Zanzibar vimechangia.”

Bimani alisema kwa thamani yoyote hakuna asiyeweza kubaini umuhimu wa hali ya amani na utulivu, na madhara ya kukosekana kwake, hasa katika visiwa hivyo vya Unguja na Pemba ambavyo vimewahi kuelemewa athari kubwa ya machafuko kwa muda mrefu.

“Chama cha Wananchi (CUF), kama sehemu muhimu ya umma wa Watanzania hakiwezi kukaa kimya kutokana na mwelekeo mzima wa hali tete ya amani katika nchi, ingawa ni dhahiri wapo baadhi ya watu wasioitakia mema Zanzibar wakibainika kufurahia mazingira hayo, kwa maslahi binafsi, na pia kutoa kauli za kutatanisha za kisiasa.

Chama cha CUF kinatoa wito kwa wananchi wote kuwa watulivu, wavumilivu na kuitumia fursa ya kutoa mawazo yao bila ya jazba, pamoja na kutowanyima wengine nafasi ya kuwasilisha mitazamo yao,” alisema.

Bimani alisema vitendo vya watu wachache kuchoma makanisa na kuharibu mali za watu ni vya uvunjifu wa sheria na kinyume cha utamaduni wa Kizanzibari na kutaka uchunguzi wa kina ufanyike na waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria, bila uonevu wala upendeleo.

“Tahadhari iwepo ya kuepuka matumizi ya mabavu yanayoweza kuleta hamasa kwa wananchi, hatimaye ikachochea vitendo vya hujuma dhidi ya watu na mali zao, na pia kuepuka tabia isiyokuwa ya haki, ya kuwabambikizia kesi wananchi,” alisema.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepiga marufuku majukwaa ya kidini kutumika kama uwanja wa kisiasa na viongozi watakaofanya hivyo watakamatwa mbele ya wafuasi wao ili kuimarisha amani na umoja wa kitaifa wa Zanzibar.

Tamko hilo lilitangazwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed, alipokuwa akizungumza na viongozi wa dini wakiwemo wachungaji, maaskofu na uongozi kutoka ofisi ya Mufti katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God liliopo Kariakoo, ambalo lilichomwa moto katika vurugu hizo.

“Serikali tumekosea kuwaachia watu, na wametumia kisingizio cha dini na kugeuza uwanja wa siasa, kama wameshindwa kutekeleza majukumu yao kama walivyoomba katika usajili wao, basi waingie katika ulingo wa siasa badala ya kutumia kivuli cha dini,” alisema.

Katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema, Waziri Aboud alisema:

“Mikusanyiko bila ya kibali marufuku, tumezaliwa siku moja na tutakufa siku moja, hakuna haja ya kutishana, atakayefanya mkutano au maandamano bila ya kibali cha Polisi, Serikali inaliagiza jeshi la Polisi kumkamata kiongozi yeyote hatutamuogopa mtu atakayevunja sheria na kuhatarisha amani ya nchi yetu.”

NYUMBA ZA IBADA KULINDWA

Waziri Aboud alisema kuanzia sasa suala la ulinzi katika nyumba za ibada halina mjadala ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unazingatiwa na kuwataka viongozi hao wa dini kuwa wavumilivu wakati serikali ikiendelea kulitafutia ufumbuzi suala hilo ikiwemo kuliagiza Jeshi la Polisi kuwatafuta wahusika na kuwafikisha katika mkono wa sheria.

Kwa upande wake, IGP Said Mwema alisema watu 76 tayari wamekamatwa na hadi jana 73 walikuwa wamekwisha kufikishwa mahakamani.

Alisema Jeshi hilo limeyapokea maagizo ya Serikali ya Zanzibar ya kuhakikisha nyumba za ibada zinapatiwa ulinzi na kuongeza kuwa Jeshi lake halitakubali vitendo vya uvunjifu wa amani viendelee.

“Polisi tunaendelea kuimarisha doria katika kila kanisa na maeneo muhimu ili kuzuia mwenendo ambao umekuwa ukitokea, tunawaomba viongozi wa dini na wananchi kusaidia kutoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa wahalifu,” alisema IGP Mwema.

KAULI ZA VIONGOZI WA DINI

Naye kiongozi mwandamizi kutoka ofisi ya Mufti wa Zanzibar, Sheikh Omar Jongo, alisema Waislamu hawahusiki na vurugu hizo kwa vile wamekuwa wakiishi na Wakiristo kama ndugu kwa miaka mingi.

Sheikh Jongo alisema yeye mwenyewe alikumbana na msukosuko akiwa na chombo cha moto aina ya Vespa ambapo vijana waliokuwa wakifanya vurugu hizo walimnyang’anya pikipiki na ‘kumpiga mtama, kabla ya kuokolewa na watu wanaomfahamu huku polisi wakitazama.

“Kwa niaba ya Waislamu, naomba kueleza kuwa hawahusiki na vurugu hizi, hata kwenye Qur’ an takatifu inatueleza, haiwezekani Waislamu wavunje baa na kuanza kunywa pombe, Uislamu hauruhusu kunywa pombe, sasa vipi waumini wavunje baa, waibe na kunywa pombe tena hadharani?” alihoji Sheikh Jongo.

Alisema viongozi wa dini wamefanya kazi kubwa iliyofanikisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kurejesha amani baada ya machafuko ya Januari 26 na 27, 2001, kupitia kamati ya pamoja ya amani ya viongozi wa dini, hivyo haingii akilini kwa viongozi hao hao wa dini kuchochea vurugu.

Naye Makamu Mkuu Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God, Dk. Magnus Mhiche, alisema hujuma dhidi ya makanisa ya Zanzibar zilianza kufanyika tangu mwaka 2011 na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi ya wahusikaa.

“Ombi langu kwa viongozi wa serikali tunapochelewa kuchukua hatua ni sawa na methali ya usipoziba ufa utajenga ukuta, ndiyo maana tukaanza kupatwa na wasiwasi kuwa wahuni wamefikia kuwa na nguvu kuliko serikali, lakini tumefarijika kwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali baada ya matukio hayo,” alisema Dk. Mhiche.

Askofu wa TAG, Dickson Kaganga, aliitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu matukio yaliyojitokeza kwa vile yanaweza kuzorotesha umoja wa kitaifa.

Naye, Askofu wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Zanzibar, Michael Hafidh, alisema maaskofu na makatibu wakuu wa makanisa kutoka Zanzibar na Tanzania Bara watakutana leo Zanzibar kujadili mambo yaliyojitokeza na kusababisha makanisa matatu kuchomwa moto Zanzibar na mali nyingine kuharibiwa.

Alisema kikao hicho kitatoka na msimamo wa pamoja na wataomba kukutana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ili kujadili mustakabali wa Zanzibar, ombi ambalo lilikubaliwa na Waziri Aboud, ambaye aliahidi kuwasilisha ombi hilo kwa Rais.

UTULIVU WAREJEA

Shughuli za kiuchumi jana mchana zilikuwa zimerejea katika hali ya kawaida huku doria zikiwa zimeimarishwa na vikosi vya ulinzi ikiwemo askari wa JKU, KVZ, wakiongozwa na Jeshi la Polisi.

Aidha, barabara nyingi zilizokuwa zimefungwa zilianza kufunguliwa na ulinzi kuwekwa katika vituo vya mafuta na makanisa.

Add a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

`
Design By : Tanzania Servers Technology