CCM, Chadema Utata Mkali

Posted on Oct 30 2012 - 1:05pm by Mwemutsi Erick

Matokeo ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 29 Tanzania Bara, yamezua malumbano makubwa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Malumbano hayo yameibuka baada ya CCM kutaka Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa ajiuzulu kwa madai ya kushindwa kwa wagombea wote wa chama hicho aliowafanyia kampeni katika uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita.

Hata hivyo, wakati CCM ikimtaka Dk. Slaa kujiuzulu kwa sababu hizo, Chadema nayo imemtaka Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, pamoja na viongozi wote wa CCM ngazi ya taifa kujiuzulu, kwa madai kwamba, ushindi ilioupata katika uchaguzi huo umepatikana kwa kutumia mbinu chafu.

CCM ilitoa kauli hiyo kupitia Nape alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati Chadema ilitoa kauli hiyo kupitia Mwenyekiti wa Baraza lake la Vijana (Bavicha), John Heche, alipozungumza kwa njia ya simu jana.

KAULI ZA CCM

Wa kwanza kutoa kauli hiyo alikuwa Nape, ambaye alisema umefika wakati sasa kwa Dk. Slaa kuwaachia vijana waipiganie Chadema, kwa kuwa kampeni zilizoongozwa naye kuwanadi wagombea udiwani kupitia chama hicho katika kata zilizoko Kanda ya Ziwa, zimesababisha kuangushwa katika uchaguzi huo.

Nape alidai mbali na Dk. Slaa, pia Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, licha ya kutumia gari la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwanadi wagombea kupitia chama hicho katika kata zilizoko Kanda ya Kusini, ameambulia patupu kwani wagombea hao nao pia wameangushwa katika kinyang’anyiro hicho.

Alisema pia matokeo ya uchaguzi huo katika kata zilizoko wilaya za Bagamoyo, mkoani Pwani na Liwale, mkoani Lindi, Chadema imeshika nafasi ya tatu.

“Watanzania wamezikataa aina ya siasa zinazofanywa na Chadema pamoja na uongo unaofanywa na viongozi wake,” alisema Nape na kuongeza:

“Dk. Slaa anaongea uongo ndiyo maana watu wamewakataa wagombea aliowanadi. Aliwahi kusema kuwa kuna mtoto wa kigogo amekamatwa na dawa za kulevya China wakati si kweli.”

Nape alisema matokeo ya uchaguzi huo yanaifanya kaulimbiu ya Chadema kubadilika; badala ya kuwa Movement for Change (M4C), kwa maana ya “Vuguvugu la Mabadiliko”, sasa imewe Movement for Death (M4D) akimaanisha “Vuguvugu la Kifo.”

Alisema ushindi wa CCM katika kata 22 kati ya kata 29, ni uthibitisho tosha kwamba sera na wagombea wa chama hicho wanakubalika, kwani imeshinda, huku ikiwa katika changamoto ya uchaguzi wa ndani ya chama.

Kata hizo 29 na halmashauri zao kwenye mabano ni Bangata (Arusha), Daraja Mbili (Arusha), Msalato (Dodoma), Mpwapwa (Mpwapwa), Magomeni (Bagamoyo), Lwezera (Geita) Bugarama (Kahama), Mwananza (Shinyanga) na Vugiri (Korogwe).

Nyingine ni Tamota (Lushoto), Makata (Liwale), Mnero na Miembeni (Nachingwea), Mlangali (Ludewa), Luwumbu (Makete), Mpepai (Mbinga), Mletele (Songea), Ipole na Kiloleli (Sikonge) na Miyenze (Tabora).

Kata nyingine ni Karitu (Nzega), Mpapa na Myovizi (Mbozi), Lubili (Misungwi), Kilema Kusini (Moshi), Nanjara/Neha (Rombo), Mtibwa (Mvomero), Mahenge (Ulanga), Likokona (Nanyumbu) na Kitangiri (Newala).

Kati ya kata hizo 29, Chadema ilishinda katika kata tano, wakati Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Tanzania Labour (TLP) kila kimoja kilishinda kata moja moja.

Nape alisema kushindwa kwa CCM katika kata hizo, kumetokana na changamoto mbalimbali zinazokikabili chama hicho, ikiwamo kusimamisha wagombea wasiokubalika, migogoro ndani ya chama na chama kushiriki uchaguzi huo huku kikiwa na uchaguzi wake wa ndani ambako nguvu kubwa iliwekwa huko.

Hata hivyo, aliwashukuru wananchi waliowachagua wagombea wa CCM na kusema: “Katika kata 29, kushinda kata 22 si jambo la mchezo.”

Alisema katika uchaguzi uliofanyika katika kata zilizoko wilaya ya Misungwi na Geita, wafuasi wa Chadema waliokutwa wakigawa chumvi kwa wapigakura, lakini mbinu yao hiyo ilifeli, baada ya kuzuiwa kufanya kampeni hiyo chafu.

Nape alisema vurugu zote zilizotokea katika uchaguzi huo katika baadhi ya maeneo zilitokana na baadhi ya watu kukataa matokeo na kusema CCM inalaani vikali vurugu hizo.

Alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa vichocheo vya vurugu na kutolea mfano wa vurugu zilizowahi kutokea katika mikoa ya Singida, Morogoro, Arusha na Iringa, ambako kote huko zilisababisha mauaji ya watu mbalimbali.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wananchi kukataa siasa za fujo na kuitaka Chadema kujenga utamaduni wa kukubali matokeo na si kuanzisha vurugu.

MAJIBU YA CHADEMA

Wakati Nape akisema hayo, Heche alisema wanaopaswa kujiuzulu ni Nape na uongozi wote wa ngazi ya juu wa CCM kutokana na kutumia mbinu chafu kushinda uchaguzi huo.

Heche alisema CCM katika uchaguzi huo ilitumia rushwa kama ilivyofanya hivyo katika uchaguzi wake wa ndani kwa nyakati tofauti hivi karibuni.

Alisema kutumika kwa rushwa katika uchaguzi wa CCM, kumethibitishwa hata na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Rais Jakaya Kikwete.

Heche alidai kwa kuwa CCM imethibitika kutumia rushwa na kutokana Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) kuwa dhaifu katika kushughulikia tatizo hilo, chama hicho hakina sababu yoyote ya msingi ya kujisifia kwamba kimeshinda uchaguzi wakati mazingira ya ushindi wao yanawasuta.

Alidai mbali na kutumia rushwa, CCM pia ilitumia Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kuwatisha wapigakura kwa kutangaza hali ya hatari baada ya watu wanaosadikiwa kuwa ni walinzi wa chama hicho maarufu kama ‘Green Guard’ kutuhumiwa kuua baadhi ya watu.

Heche alidai katika kutangaza hali hiyo, Jeshi hilo liliwataka wananchi kutokwenda kupiga kura, hali ambayo iliipa CCM mwanya wa kushinda kirahisi, kinyume cha hali halisi.

Hata hivyo, alisema CCM wanapaswa kurudi na kujiuliza tatizo linaloikabili, kwani kwa mara ya kwanza Chadema imeweza kusimamisha wagombea katika kata zote 29 na kuvunja mwiko wa zamani wa CCM katika uchaguzi huo kupita bila kupingwa.

Alisema pia katika kata zote 29, Chadema imefanikiwa kuongeza kura zaidi ya zile ilizopata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Heche alisema vilevile, kata mbili za Nanjara/Neha, mkoani Arusha na Mtibwa, mkoani Morogoro zilizokuwa kwenye himaya ya Chadema, zote wameshinda na kuongeza kata nyingine tatu zilizokuwa chini ya himaya ya CCM.

Alizitaja kata hizo tatu kuwa ni pamoja na ile ya Daraja Mbili, iliyoko mkoani Arusha, Ludewa, mkoani Iringa, Iringa na Kiloleli (Sikonge), mkoani Tabora.

“Hivyo, kujisifu kwamba ulikuwa na watoto kumi, wawili wakafa unafurahi watoto wako kufa?” alihoji Heche.

Alisema pia faida nyingine waliyoipata kinyume cha inavyokejelewa na CCM, ni kwamba, katika kipindi chote cha uchaguzi huo, Chadema ilifanikiwa kuvifikia vijiji 116, ambako walitumia fursa hiyo kuimarisha chama na kufungua matawi mapya ya chama.

“Kwa hiyo, kama ni kujiuzulu, basi Nape na uongozi wa CCM ndiyo wanaopaswa kujiuzulu,” alisema Heche.

RPC MBEYA ANENA

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, alipoulizwa nasi kuhusu madai ya Polisi kutumika kuwatisha wapiga kura, alisema mtu aliyetoa madai hayo ndiye anayeweza kuyathibitisha ikiwa ni pamoja na kueleza vizuri na si yeye.

“Mimi ninachoweza kusema ni kwamba, huo ni uongo na ni uzushi, kwisha, basi,” alisema Kamanda Athumani.